Storm FM
Storm FM
8 August 2026, 12:27 pm

Pampu hizo zimegawanywa katika halmashauri tano ambapo Bukombe imepata 16, Chato 41, Geita DC 50, Mbogwe 20 na Nyang’hwale 14.
Na Mrisho Sadick:
Serikali kupitia tume ya taifa ya umwagiliaji imekabidhi pampu 141 za umwagiliaji zenye thamani ya shilingi bilioni moja kwa vikundi vya wakulima mkoani Geita hatua hiyo ikilenga kuongeza uzalishaji wa mazao na kuwawezesha wakulima kulima mwaka mzima.

Mhandisi kutoka Tume ya taifa ya Umwagiliaji Mkoa wa Geita Boniface Mkita amesema jumla ya wakulima 1,389 watanufaika na mpango huo wakiwemo wanawake 369 na wanaume 1,020 nakwamba Pampu hizo zitatumika katika maeneo yenye vyanzo vya maji ikiwemo mito na maziwa na zina uwezo wa kumwagilia zaidi ya ekari 20 kwa saa moja.
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Paskas Muragili amesema kupitia mpango huo uzalishaji wa mahindi unatarajiwa kuongezeka kutoka tani moja hadi tani 2.5 kwa ekari huku akisisitiza walengwa kuzitunza ili zitumike kwa muda mrefu.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Mohamed Gombati amesema katika mpango huo ekari zaidi ya 2,092 zinatarajiwa kumwagiliwa nakwamba matumizi ya pampu hizo yataongeza uzalishaji wa mbogamboga kutoka tani sita hadi tani 10 kwa ekari moja.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale amesema pampu hizo zitawawezesha wakulima kuzalisha kwa mwaka mzima bila kutegemea mvua.