Storm FM
Storm FM
1 September 2026, 1:40 pm

Madiwani wameendelea kusisitiza kuwa hatua za haraka zinahitajika hususan kabla na wakati wa msimu wa mvua ili kuzuia barabara kukatika, kuathiri usafiri wa wananchi na kusababisha usumbufu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Na Mrisho Sadick:
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita wameitaka Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA kuchukua hatua za haraka kukarabati na kuboresha miundombinu ya barabara kabla ya kuanza kwa msimu wa mvua kubwa ikiwemo mvua za El Niño zinazoweza kuongeza madhara kwa wananchi.
Madiwani hao wameibua hoja hiyo wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Geita wakieleza kuwa baadhi ya barabara katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo zimeharibika na kuhatarisha usafiri wa wananchi pamoja na shughuli za kiuchumi.

Aidha madiwani hao wameitaka TARURA kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara kinyume na matakwa na makubaliano yaliyowekwa kwenye mikataba wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi hiyo inatekelezwa kwa viwango vinavyokubalika.
Kutokana na hoja hizo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Jumanne Sengo Misungwi ameiagiza TARURA kuandaa majibu ya kina kuhusu changamoto za barabara zilizobainishwa na madiwani pamoja na hatua zinazochukuliwa kuzitatua.

Mwenyekiti huyo amesema majibu hayo yanapaswa kuwasilishwa katika kikao kijacho cha Baraza la Madiwani ili kuwezesha ufuatiliaji wa utekelezaji wa maagizo hayo.