Storm FM

Madiwani waridhia kukamilisha uwanja wa Magogo kwa fedha za ndani

22 August 2026, 12:35 am

Picha ya baadhi ya madiwani wakiwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi Agosti 21, 2026. Picha na Ester Mabula

Ujenzi wa uwanja huo awali ulikuwa chini ya fedha za uwajibikaji wa Kampuni kwa jamii (CSR) zinazotolewa na kampuni ya GGML ambapo baraza la madiwani limeridhia fedha hizo zitumike kwenye miradi mingine ya maendeleo.

Na: Ester Mabula

Baraza la madiwani la halmashauri ya manispaa ya Geita limeadhimia kukamilisha uwanja wa mpira wa miguu uliopo eneo la Magogo, kata ya Bombambili manispaa ya Geita kwa fedha za mapato ya ndani ya halmashauri.

Maazimio hayo yamefikiwa katika kikao cha baraza la madiwiani kilichoketi Agosti 21, 2026 ambapo madiwani wameeleza hatua hiyo inafuatia kusuasua kwa mradi huo ambao umeanza kujengwa kwa zaidi ya miaka mitatu.

Wakizungumza wakati wa kikao hicho, madiwani wameeleza kuwa dhamira ya wananchi wa Geita si tu kushsuhudia timu yao ya Geita Gold FC ikicheza katika manispaa ya Geita bali pia hatua hiyo itaendelea kukuza uchumi wa manispaa kwa ujumla.

Sauti ya madiwani

Akizungumza Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mhandisi Chacha Wambura amesema kuna baadhi ya halmashauri hazina wawekezaji ikiwemo migodi na kwamba ni wakati wa kuangalia vyanzo vingine vya kukamilisha mradi huo huku Mstahiki Meya Leornad Bugomola akisema lengo lao si kuomba fedha za mgodi bali mwekezaji awajibike kwa mujibu wa sheria.

Sauti ya mbunge na mstahiki meya
Mstahiki meya manispaa ya Geita Leonard Bugomola akizungumza wakati wa kikao cha baraza. Picha na Ester Mabula

Akisoma maadhimio ya kikao hicho Naibu mstahiki meya wa manispaa ya Geita amesema mchakato wa kukamilisha mradi huo unaanza mara moja ndani ya mwaka huu wa fedha 2026/2027 ili kuhakikisha azma ya manispaa ya kuwa na kiwanja cha michezo inakamilika kama ilivyokusudiwa.

Sauti ya naibu mstahiki meya
Naibu mstahiki meya Elias Ngole akisoma taarifa za maazimio ya kikao cha baraza la madiwani. Picha na Ester Mabula