Storm FM
Storm FM
22 September 2026, 6:55 pm

“Miongoni mwa mambo niliyojifunza kupitia ziara hii ni umuhimu wa kuunganisha teknolojia na usafirishaji ili kuongeza ufanisi, kuboresha huduma na kufungua fursa zaidi za kiuchumi hususani kwa vijana” – Manjale Magambo
Na: Mwandishi wetu
Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa chama cha Mapinduzi (UVCCM) mkoa wa Geita, Manjale Magambo, ametembelea kiwanda cha kutengeneza mabasi cha Yutong, kilichopo Zhengzhou nchini China, kwa mwaliko rasmi, ikiwa ni sehemu ya kujifunza mbinu na teknolojia zinazoweza kusaidia kukuza sekta ya usafirishaji na kuchochea shughuli za kiuchumi.
Magambo amefanya ziara hiyo kwa lengo la kujifunza namna nchi hiyo inavyotumia sekta ya usafirishaji kama sehemu ya maendeleo ya uchumi, pamoja na kupata uelewa kuhusu teknolojia na mifumo mbalimbali inayotumika katika uzalishaji wa mabasi.
Akiwa katika kiwanda hicho, Magambo amepata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazofanyika katika uzalishaji wa mabasi, hatua inayompa nafasi ya kufahamu kwa karibu teknolojia na mbinu zinazotumika katika sekta hiyo.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda hicho, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Geita, Manjale Magambo, amesema ziara hiyo imempa fursa ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu maendeleo ya sekta ya usafirishaji, hususan matumizi ya teknolojia katika uzalishaji wa mabasi na namna sekta hiyo inavyoweza kuchangia ukuaji wa uchumi.
Magambo amesema uzoefu alioupata nchini China ni muhimu katika kuwasaidia vijana kuelewa fursa zilizopo katika sekta ya usafirishaji, ikiwemo teknolojia, uwekezaji, ajira na ujasiriamali.