Storm FM
Storm FM
19 October 2026, 2:31 pm

Baada ya kushambuliwa marehemu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa matibabu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Na Mrisho Sadick:
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linafanya uchunguzi wa kifo cha Dotto Alex (19) aliyefariki dunia Oktoba 7, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza baada ya kupigwa kichwani kwa kitu butu huko Lwamgasa, Wilaya ya Geita.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 6, 2026 majira ya saa saba usiku marehemu akiwa pamoja na watu wengine katika burudani ya disko vumbi nyumbani kwa mganga wa kienyeji anayetambulika kwa jina moja la Samwel.

Wakati burudani ikielekea ukingoni, alijitokeza mwanaume mmoja ambaye alianza kuwatawanya watu waliokuwa eneo hilo kabla ya kumpiga marehemu kichwani kwa kitu butu na kutoroka eneo la tukio.
Baada ya kushambuliwa, marehemu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita kwa matibabu na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambako alifariki dunia Oktoba 7, 2026 wakati akipatiwa matibabu.

Jeshi la Polisi linafanya uchunguzi wa tukio hili, mwili wa marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya taratibu za mazishi baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kitaalamu huku msako wa kumtafuta mtuhumiwa ukiendelea.
Baba mzazi wa kijana huyo Alex Mipawa ameiomba serikali kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa wa tukio hilo huku mdogo wa marehemu ameeleza kuwa kaka yake alipigwa kisha kuanguka chini na mtuhumiwa kutokomea kusiko julikana.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linatoa wito kwa mtu yeyote hasa waliokuwa eneo la tukio mwenye taarifa za mtuhumiwa azitoe katika kituo cha Polisi au kwa viongozi wa Serikali katika eneo analoishi ili hatua za kisheria zichukuliwe.