Storm FM

TCB yatenga bilioni 15 ya mikopo kwa wafanyabiashara Geita

3 September 2026, 6:32 pm

Mkuu wa wilaya ya Chato akiwa na viongozi mbalimbali azindua Tawi la Bank ya TCB Chato mjini. Picha na Mrisho Sadick

Wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima pamoja na wachimbaji wa dhahabu wametakiwa kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa

Na Mrisho Sadick:

Benki ya TCB imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara, wakulima na wachimbaji wa madini ya dhahabu katika Wilaya ya Chato mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuwawezesha wananchi kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuongeza kipato.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Wateja Binafsi na Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati wa TCB Bi Lilian Mtali leo Septemba 03,2026 wakati wa uzinduzi wa tawi jipya la benki hiyo mjini Chato.

Amesema jengo la tawi hilo lina mazingira mazuri na rafiki kwa utoaji wa huduma, yanayoakisi dhamira ya Tanzania ya kuendelea kuimarisha huduma za kifedha na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Viongozi wa Bank ya TCB wakiwa na Mkuu wa wilaya ya Chto katika uzinduzi wa tawi la bank hiyo. Picha na Mrisho Sadick

Mtali ameongeza kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita mali za TCB zimefikia Shilingi trilioni 2.5 huku mikopo kwa wateja ikifikia Shilingi trilioni 1.6 na amana za wateja kufikia Shilingi trilioni 1.73.

Aidha TCB ni benki ya tatu nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya matawi ikiwa na jumla ya matawi zaidi ya 84 huku pia ikiwa imejiunga na mifumo yote ya serikali inayohusiana na huduma za kifedha.

Muonekano wa tawi jipya la Bank ya TCB lililozinduliwa Chato mjini. Picha na Mrisho Sadick

Baada ya uzinduzi wa tawi hilo Mkuu wa Wilaya ya Chato Louis Bura amewataka wananchi kutumia fursa hiyo kukuza mitaji na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi, amesisitiza kuwa TCB, ambayo sehemu kubwa ya umiliki wake ipo serikalini ina nafasi muhimu katika kuwawezesha wananchi kupata huduma za kifedha.

Amewahimiza wafanyabiashara wadogo na wa kati, wakulima pamoja na wachimbaji wa dhahabu kutumia mikopo hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuongeza uzalishaji na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.