Storm FM

Mwanamke amtelekeza mume wake baada ya kupata ulemavu wa macho Balatogwa

15 September 2026, 4:25 pm

Muonekano wa picha ya mwanamke kumtelekeza mume wake baada ya kupata ulemavu wa macho. Picha na Mtandao

Hali ya Mazoea imeibua wito kwa jamii kuendelea kuimarisha mshikamano na kujali watu wenye ulemavu, kwa kuhakikisha wanapata msaada na fursa za kuishi maisha yenye utu na heshima.

Na Mrisho Sadick:

Mwanaume aliyefahamika kwa jina la Mazoea Myombya (61) mkazi wa Kitongoji cha Balatogwa Kata ya Mwabaluhi Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza ametelekezwa na mke wake baada ya kupata ulemavu wa macho unaomfanya ashindwe kuendelea na shughuli zake za kila siku kama awali.

Akizungumzia hali yake Mazoea amesema kwa sasa anakabiliwa na changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo ukosefu wa mahitaji muhimu ya msingi, hususani chakula, kutokana na kushindwa kujitegemea kikamilifu baada ya kupoteza uwezo wa kuona ambapo amesema hali hiyo imemfanya kukumbwa na maisha magumu na kuhitaji msaada wa ndugu majirani pamoja na watu wenye moyo wa huruma ili aweze kupata mahitaji muhimu na kuendelea na maisha.

Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Balatogwa wameeleza kusikitishwa na kitendo cha mwanamke huyo kumtelekeza mume wake wakati akikabiliwa na changamoto ya kiafya, wakisisitiza umuhimu wa wanandoa kusimama pamoja katika nyakati ngumu na nyakati za furaha.

Wananchi hao pia wamewataka wanandoa, hususani wanawake, kutochukulia changamoto za kiafya au ulemavu kama sababu ya kuvunja mshikamano wa kifamilia, bali kuwa na moyo wa uvumilivu, upendo na kusaidiana.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kitongoji cha Balatogwa Safari Shigemelo amekiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa mwanaume huyo ametelekezwa na mke wake baada ya kupata ulemavu wa macho huku akiwataka wanandoa kuwa na uvumilivu na kuheshimiana katika ndoa nakwamba changamoto za kiafya na kiuchumi zinaweza kumkuta mtu yeyote na hivyo ni muhimu wanandoa kusimama pamoja wakati wa matatizo.

Aidha amewataka viongozi wa eneo hilo ndugu marafiki na wananchi wenye uwezo kushirikiana kumsaidia Mazoea kupata mahitaji ya msingi na huduma muhimu, huku akisisitiza kuwa msaada wa jamii ni muhimu kwa watu wanaokabiliwa na changamoto za ulemavu.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick