Storm FM

Wadaiwa sugu wa mapato ya serikali kusakwa Geita

2 July 2026, 6:48 pm

Mkuu wa mkoa wa Geita wa pili kutoka kushoto akiwa kwenye kikao cha baraza la madiwani Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, halmashauri imeweka mkakati wa kuwatambua wadaiwa sugu na kufuatilia malipo yao kwa wakati, sambamba na kuongeza uwajibikaji kwa watendaji wanaosimamia vyanzo vya mapato.

Na Mrisho Sadick:

Serikali mkoani Geita imeziagiza halmashauri zote za wilaya kuhakikisha zinaandaa utaratibu madhubuti wa kuwabaini wadaiwa sugu wa mapato ya serikali ili kuwezesha ukusanyaji wa madeni hayo kwa wakati na kuongeza ufanisi wa mapato ya ndani.

Maagizo hayo yametolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita Herman Matemu wakati wa kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale cha kujadili taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

Madiwani na viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani wilaya ya Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji katika ukusanyaji wa mapato kutoka kwenye vyanzo vyote vilivyoidhinishwa kwenye bajeti akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame amewataka watendaji wa halmashauri hiyo kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uwajibikaji ili kupunguza na ikiwezekana kuondoa kabisa hoja zitakazojitokeza katika ukaguzi ujao wa CAG.

Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Nyang’hwale wakiwa kwenye kikao cha baraza cha CAG. Picha na Mrisho Sadick

Akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale Husna Toni amesema kuwa licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi ya ukaguzi kwa mara ya sita mfululizo itaendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo na ushauri uliotolewa ili kuboresha zaidi usimamizi wa fedha za umma na kuimarisha utendaji wa halmashauri.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyang’hwale John Isack amesema ataendelea kusimamia kwa karibu ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na kuwawajibisha watendaji wa serikali ili kuhakikisha kila mmoja anatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick