Storm FM
Storm FM
6 July 2026, 3:52 pm

Changamoto ya walanguzi wa mazao kwenda moja kwa moja mashambani imegeuka mwiba mchungu kwa wakulima wilayani Mbogwe huku wakidai kupata hasara nakuiomba serikali kuingilia kati.
Na Mrisho Sadick:
Wakulima wa Kata ya Ilolangulu Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita wameiomba Serikali kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao na kujenga maghala ya kuhifadhia mazao ili kuwaepusha na changamoto ya wafanyabiashara wanaokwenda kununua mazao moja kwa moja mashambani kwa kutumia vipimo visivyo rasmi.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima hao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Simon Samike ambaye ni mkulima wa mpunga, amesema uwepo wa vituo rasmi vya ununuzi wa mazao utasaidia kuondoa unyonyaji unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara wanaofika vijijini na kununua mazao kwa bei na vipimo visivyozingatia taratibu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Wakili Edwin Bayona amesema Serikali inatambua uwepo wa changamoto hiyo ikiwemo wafanyabiashara kutumia vipimo vyao wenyewe wakati wa ununuzi wa mazao nakwamba Halmashauri imeendelea kufanya doria katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha wanunuzi na walanguzi wa mazao wanafuata sheria.


Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amewaagiza watendaji wa vijiji na kata wilayani Mbogwe kuhakikisha wanatenga na kuanzisha vituo rasmi vya ununuzi wa mazao katika maeneo yao hatua hiyo itawazuia wanunuzi kwenda kununua mazao moja kwa moja mashambani.