Storm FM
Storm FM
2 July 2026, 11:21 am

Mamlaka ya mapato nchini Tanzania ilianzishwa rasmi Julai 01, 1996 ambapo imetimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya mambo mbalimbali kwenye jamii sambamba na kuwatambua walipa kodi wanaofanya vizuri.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetunukiwa Tuzo mbili za Rais za Walipakodi, ikitambuliwa kuwa mlipakodi namba moja nchini na kampuni inayozingatia kwa kiwango cha juu zaidi sheria za kodi kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Tuzo hizo zilitolewa katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yaliyofanyika Jumanne katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, Dar es Salaam, chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu isemayo “Miaka 30 ya TRA, Mlipakodi Shujaa, Tanzania Inajitegemea,” na yaliwakutanisha viongozi wa Serikali, wafanyabiashara pamoja na wadau mbalimbali kwa lengo la kutambua walipakodi wanaotekeleza wajibu wao kwa uadilifu na hivyo kuchangia utoaji wa huduma za umma, maendeleo ya taifa na agenda ya kujitegemea.
Tuzo hizo zilipokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, akiwa ameambatana na Makamu wa Rais wa Kampuni anayesimamia Uendelevu na Ushirikishwaji wa Wadau, Simon Shayo, pamoja na Meneja Mwandamizi wa Migogoro ya Kodi, Godvictor Lyimo.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Ashraf Suryaningrat alisema heshima hiyo ni matokeo ya juhudi za pamoja za wafanyakazi, wasambazaji na wadau wote wanaoshirikiana na kampuni.
Alieleza kuwa tuzo hizo zina umuhimu mkubwa katika muktadha wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeitambua sekta ya madini kuwa moja ya nguzo kuu za kufanikisha azma ya Tanzania kuwa na uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Kwa mujibu wa Dira hiyo, sekta ya madini inatarajiwa kuendelea kuchochea ajira, kuongeza mapato ya mauzo ya nje, kuimarisha viwanda vinavyotegemea madini pamoja na kuongeza thamani ya rasilimali za nchi. Kutambuliwa kwa GGML kama mlipakodi bora na kampuni inayozingatia sheria za kodi kunadhihirisha mchango wa uchimbaji madini unaowajibika katika kufanikisha ajenda hiyo ya kitaifa.
Tangu kuanza shughuli zake nchini, GGML imechangia zaidi ya dola za Marekani bilioni 3.7 kupitia kodi mbalimbali kwa Serikali ya Tanzania.
Kwa sasa, GGML inaajiri zaidi ya watu 7,000, ambapo asilimia 98 ni Watanzania. Kampuni hiyo pia inashirikiana na zaidi ya kampuni ndogo na za kati 600 za Kitanzania katika mnyororo wake wa ugavi na mtandao wa biashara, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera na kanuni za maudhui ya ndani (Local Content) nchini Tanzania.