Storm FM
Storm FM
15 May 2026, 5:39 pm

Halmashauri ya manispaa ya Geita inawezesha ujenzi wa mradi mkubwa wa GEDECO Tower ambao unatarajiwa kuongeza mapato na kuchochea maendeleo kwa wakazi wa Geita.
Na: Ester Mabula
Halmashauri ya Manispaa ya Geita imeanza rasmi ujenzi wa mradi mkubwa wa kitega uchumi cha GEDECO Tower utakaokuwa na ghorofa 8 ukigharimu kiasi cha jumla ya shilingi bilioni 13, ambapo ujenzi wake unatekelezwa kikamilifu kwa kutumia mapato ya ndani ya halmashauri.
Mkurugenzi wa manispaa ya Geita Ndg. Yefred Myenzi amesema ndani ya jengo hilo kutakuwa na huduma mbalimbali akisema mradi huo utakuwa chachu ya kuongeza uchumi kwa ujumla.
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba ameipongeza Halmashauri ya manispaa ya Geita kwa kuanzisha mradi huo akisema ukuaji wa manispaa unaendana sambamba na ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Mstahiki Meya wa manispaa ya Geita Leonard Bugomola amesema lengo lao ni kukamilisha mradi mapema zaidi tofauti na matarajio ya miaka mitatu huku baadhi ya wananchi waliopata fursa ya vibarua katika mradi huo wameeleza namna ambavyo wananufaika,
Kukamilika kwa mradi huu kutaleta faida kubwa ikiwemo kuongeza vyanzo endelevu vya mapato ya ndani kupitia kodi ya pango na kukuza biashara.
