

27 May 2025, 2:43 pm
Uvumilivu wa migogoro ya madaraka umewashindwa wananchi nakuamua kumuangukia mkuu wa mkoa kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo kwenye kijiji chao.
Na Mrisho Sadick:
Wakazi wa Kijiji Cha Saragulwa wilaya ya Geita Mkoani Geita wameiomba serikali kuingilia kati Sakata la wenyeviti wanaochaguliwa kwenye Kijiji hicho kutomaliza miaka mitano ya Uongozi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupinga vitendo vya Rushwa vinavyotokana na ajira za ulinzi wa Bomba la maji la Mgodi wa GGML linalopita katika eneo hilo.
Wananchi hao wametoa kilio hicho mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela aliyefika katika Kijiji hicho kukagua shughuli za maendeleo, Kusikiliza nakutatua changamoto ambapo baadhi ya wakazi wa Kijiji hicho wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kukomesha hali hiyo kwakuwa wameshindwa kufanya maendeleo kwasababu ya watu binafsi.
Mtendaji wa Kata hiyo Jonas Changanya amekiri kuwepo kwa mgogoro huo nakwamba katika maamuzi ya awali Mwenyekiti wa sasa yupo katika hati hati ya kufukuzwa kwa madai ya kupinga vitendo vya Rushwa katika mchakato wa vijana wa Kijiji hicho kuomba ajira ya ulinzi wa Bomba la maji.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amelaani vikali vitendo hivyo ambavyo vimesababisha kijiji hicho kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo ambapo ameahidi kuchukua hatua ili kukomesha tabia hiyo iliyojengeka kwa muda mrefu.