Storm FM
Storm FM
16 May 2026, 4:00 pm

Hakika msemo wa wahenga usemao ukihitaji mali basi utaipata shambani umeendelea kujidhihirisha baada ya vijana kutoka Geita kutaraji kunufaika na kilimo.
Na Mrisho Sadick:
Mbunge wa Jimbo la Geita mjini Mhandisi Chacha Wambura amewawezesha Jumla ya vijana 23 kutoka Kata za Shiloleli na Bung’hwangoko katika Manispaa ya Geita kupatiwa mafunzo ya mbinu bora za kilimo cha kisasa cha nyanya ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuwawezesha vijana kujiajiri na kupunguza changamoto ya ukosefu wa ajira kupitia sekta ya kilimo.
Vijana walioshiriki katika ziara hiyo ya mafunzo wamesema elimu waliyoipata imewapa mwanga mpya wa kuona kilimo kama ajira yenye manufaa huku wakieleza kuwa kilimo cha nyanya kinaweza kuwa chanzo kikubwa cha kipato na maendeleo endapo kitapewa msukumo na uwezeshaji wa kutosha.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mbunge wa Geita Mjini Mhandisi Chacha Wambura amesema mpango huo unalenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuwawezesha vijana kiuchumi kwa kuwapatia maarifa na mbinu za kujiajiri kupitia kilimo cha kisasa chenye tija.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mkulima wa nyanya Saidi Nkumba amesema sekta ya kilimo ina nafasi kubwa ya kuzalisha ajira kwa vijana ikiwa watazingatia matumizi ya teknolojia ubunifu na utaalamu katika uzalishaji wa mazao.

Naye Afisa Kilimo wa Manispaa ya Geita Kisomeko Alan amesema mafunzo hayo yamekuwa na manufaa makubwa kwa washiriki hasa katika kuelewa faida za kilimo cha Green House ikiwemo kuongeza uzalishaji, kupunguza matumizi ya dawa pamoja na kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.