Storm FM

Vijana zaidi ya 200 wajiunga sungusungu kulinda kijiji chao Geita

5 September 2023, 9:44 am

Baadhi ya vijana waliojiunga katika Jeshi la Jadi Buyagu Geita wakiwa katika mafunzo. Picha na Mrisho Sadick

Uhaba wa askari wa Jeshi la Polisi wilayani Geita umewaibua vijana kujiunga katika Jeshi la Jadi ili kulinda kijiji chao.

Na Mrisho Sadick:

Zaidi ya vijana 200  wa kijiji cha Buyagu wilayani Geita wamejiunga katika Jeshi la Jadi maarufu kama Sungusungu ili kupata mafunzo ya kukabiliana na vitendo vya uhalifu ikiwemo wizi wa mifugo katika eneo hilo.

Vijana hawa wazalendo wenye moyo wa nyama na damu wamechoshwa na vilio vya baadhi ya wakazi wa kijiji hicho kuvamiwa, kuibiwa mali zao na kuachwa wakiwa masikini wakutupwa wakiwa hawana mbele wala nyuma.

Wakazi wa kijiji hicho wamesifu hatua hiyo huku mwenyekiti wa Serikali ya kijiji Maneno Hassan amesema mafunzo hayo yametolewa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

Sauti ya Wananchi na Mwenyekiti

Vijana hawa wa kike na kiume wamepata mafunzo haya kwa takribani siku 45 huku wakiahidi kukilinda Kijiji hicho kwa jasho na damu.