Storm FM

Kampuni ya Blue Coast yakarabati madarasa saba

10 January 2024, 7:16 pm

Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe aliyevaa suti nyeupe akiwaongoza wananchi , wanafunzi na wadau wa elimu katika hafla ya kuzindua madarasa yaliyofanyiwa marekebisho. Picha na Mrisho Sadick

Wawekezaji wazawa waliyopo wilayani Geita wametakiwa kushirikiana na serikali kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta ya elimu kwenye maeneo waliyowekeza.

Na Mrisho Sadick – Geita

Wakazi wa Mtaa wa Nyamalembo Kata ya Mtakuja Halmashauri ya Mji wa Geita wameishukuru kampuni ya Blue Coast Investment kwa kukarabati vyumba saba vya madarasa na Ofisi mbili za walimu  katika Shule ya Msingi Nyamalembo.

Wananchi hao wametoa pongezi hizo katika hafla ya kukabidhi madarasa hayo Shuleni hapo huku wakiwaomba wawekezaji wengine katika eneo hilo kusaidia ukarabati wa majengo chakavu yaliyobaki kwenye shule hiyo.

Sauti ya wakazi wa Mtaa wa Nyamalembo

Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nyamalembo vilivyofanyiwa marekebisho. Picha na Mrisho Sadick

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyamalembo amesema kukamilika kwa ukarabati huo utaongeza ari ya wanafunzi Kujifunza huku Meneja wa Blue Coast Investment Jeremiah  Mussa akisema ukarabati huo umegharimu milioni 43.

Sauti ya Mwalimu Mkuu na Meneja wa Blue Coast

Diwani wa Kata ya Mtakuja ambae ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Geita ilipo shule hiyo Costantine Morandi amepongeza hatua hiyo huku Mkurugenzi wa kampuni ya Blue Coast Investment Athanas Inyasi amesema ataendelea kushiriki shughuli za kijamii kwakuwa serikali imeendelea kuweka Mazingira mazuri kwa wawekezaji.

Sauti ya Diwani Kata ya Mtakuja na Mkurugenzi wa Blue Coast

Mkuu wa wilaya ya Geita Cornel Magembe Sambamba nakuipongeza kampuni ya Blue Coast kwa ukarabati huo ameahidi kutoa mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya kuanza ukarabati kwenye Madarasa mengine chakavu yaliyopo kwenye shule hiyo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Geita

Baadhi ya wanafunzi wa shule ya Msingi Nyamalembo wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa madarasa. Picha na Mrisho Sadick