Storm FM
Storm FM
14 August 2026, 3:50 pm

Jumla ya watoto 300 wanatarajiwa kunufaika kupitia mpango huo wa matibabu ambapo Geita Gold Mining Limited (GGML) itafadhili jumla ya shilingi Bilioni 1.2 kwa muda wa miaka mitatu.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) zimeingia katika ushirikiano wa kimkakati (MOU) wa miaka mitatu wenye lengo la kusaidia upatikanaji wa huduma za upasuaji maalumu wa moyo kwa watoto wenye changamoto ya moyo nchini.
Kupitia makubaliano hayo yaliyosainiwa leo Agosti 14, 2026, GGML itatoa msaada wa kifedha kugharamia upasuaji wa moyo kwa watoto 100 kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitatu, ikiwa ni uwekezaji wa TZS milioni 400 kwa mwaka na hivyo kufikia uwekezaji unaotarajiwa wa jumla ya TZS Bilioni 1.2 katika kipindi chote cha miaka mitatu.
Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya JKCI Dkt. Peter Kisenge, ambaye pia ni Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo amesema magonjwa ya moyo yameendelea kusumbua watoto kwani katika watoto 100 wanaozaliwa, watoto wawili hupatikana na matatizo ya moyo na kwamba ushirikiano na GGML utasaidia kuokoa watoto wenye matatizo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema ushirikiano huo utawezesha matibabu kwa watoto 300 kote nchini huku Meneja mwandamizi wa uendelevu na mahusiano Bw. Gilbert Mworia akieleza ushirikiano huo ni wenye tija kwani utasaidia kuokoa watoto wenye changamoto ya moyo.
Ushirikiano huu unaendeleza msaada ambao GGML imekuwa ikiutoa katika huduma za matibabu ya moyo kwa watoto. Tangu Novemba 2024, GGML imekuwa ikishirikiana na JKCI na Mwaka 2025, ilitoa TZS milioni 56, ambazo zilisaidia kugharamia upasuaji wa moyo wa kuokoa maisha kwa watoto 14.
