Storm FM
Storm FM
28 August 2026, 11:38 pm

Uwekezaji kama wa Hoteli ya KER ni mfano wa namna rasilimali za mtu binafsi zinavyoweza kutumika kujenga uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.
Na Mrisho Sadick:
Mwenge wa Uhuru umekagua na kuzindua uwekezaji wa Hoteli ya KER iliyopo katika mji wa Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha uwekezaji wenye tija unaochochea maendeleo ya wananchi na huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza baada ya kukagua na kuzindua mradi huo Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 Wazo Mwang’onda amewahimiza Watanzania kujikita katika uwekezaji unaolenga kuleta maendeleo na kuboresha huduma katika maeneo yao.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii, hivyo inaendelea kuweka mazingira na sera rafiki kwa wawekezaji ili kuwawezesha kutekeleza miradi yao kwa ufanisi.

Meneja wa KER HOTEL Jastine Katunzi amesema mradi huo umegharimu zaidi ya milioni 974, ambazo zimetumika katika ujenzi wa jengo, ununuzi wa vifaa pamoja na maandalizi mbalimbali ya kuanza kutoa huduma.
Mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na umewezesha ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wananchi zaidi ya 126, hatua inayosaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.
Uzinduzi wa hoteli hiyo unaongeza fursa za huduma za malazi katika eneo la Ushirombo ambalo kwasasa limekuwa na mwingiliano mkubwa wa watu na kuchangia kukuza shughuli za biashara na utalii pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi wa eneo hilo.