

4 June 2025, 7:00 pm
Utunzaji na usafishaji wa mazingira Manispaa ya Geita umendeelea kupewa nguvu na wadau mbalimbali ili kukabiliana na changamoto ya magonjwa ya milipuko.
Na Mwandishi Ester Mabula:
Kuelekea katika kilele Cha siku ya Mazingira duniani Mgodi wa GGML kwa kushirikiana na Manispaa ya Geita Mkoani Geita imezindua kampeni maalum ya usafi wa mazingira hususani katika maeneo yenye msongamano mkubwa wa watu ikiwemo masokoni na vituo vya magari ya abiria.
Akizungumza kwaniaba ya Mgodi wa GGML Juni 03,2025 katika uzinduzi wa kampeni hiyo ulioenda sambamba na zoezi la kufanya usafi katika soko la Nyankumbu Manispaa ya Geita Elibariki Jambau kutoka idara ya mahusiano amesema katika kampeni hiyo ya usafishaji mazingira Mgodi huo umetoa vifaa vya usafi wa mazingira, ikiwemo vya kukusanyia na kuhifadhia taka, na kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii nakwamba zoezi hilo litakuwa endelevu.
Afisa mazingira Kutoka GGML Justine Fuime amesema Sheria ya uhifadhi na utunzaji wa taka inaelekeza utenganishaji wa taka taka hususani zile ngumu ambazo haziozi kwa lengo la kukabiliana na taka za plasitiki huku Afisa mazingira wa Manispaa ya Geita Sebastian Masunga amekiri kampeni hiyo ya GGML kuwa kichocheo kikubwa kwa wananchi kutambua umuhimu wa kusafisha mazingira.
Wananchi na wafanyabiashara walioshiriki katika zoezi hilo la usafi wameipongeza GGML huku wakiiomba serikali kuweka utaratibu wa kuwawajibisha baadhi ya watu wanaopuuzia suala la usafi wa mazingira katika maeneo yao ya biashara na makazi.