Storm FM
Storm FM
7 May 2026, 6:45 pm

Halmashauri inatambua nguvu kubwa inayofanywa na wananchi kwa kujenga shule shikizi na kwa bajeti ijayo tutahakikisha tunakamilisha shule zote zilizoanzishwa kwa nguvu za wananchi – Mkurugenzi Myenzi
Na: Ester Mabula
Halmashauri ya manispaa ya Geita imejipanga kukamilisha shule shikizi zinazoanzishwa kwa nguvu za wananchi ili kusaidia wanafunzi kupata elimu kwa urahisi.
Hayo yameelezwa leo Mei 07, 2026 na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya manispaa ya Geita Ndg. Yefred Myenzi wakati akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani cha kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa EPZA uliopo kata ya Bombambili manispaa ya Geita.
Mkurugenzi Myenzi amesema wanaendelea kutambua jitihada za wananchi ambao wanaanzisha ujenzi wa shule shikizi na kwamba kwa mwaka mpya wa fedha watakamilisha maboma ya shule hizo huku akieleza kuwa wameongeza bajeti kwenye elimu ili kuongeza vyumba vya madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi.

Katibu tawala wa wilaya ya Geita Bi. Lucy Beda ameipongeza manispaa ya Geita kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato na kufikia asilimia 107.
Mstahiki wa Meya wa manispaa ya Geita Leonard Bugomola amesema juhudi za kuongeza mapato ya halmashauri zinatokana na umoja na ushirikiano wa madiwani huku Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Geita Barnabas Mapande akiwapongeza viongozi wa manispaa ya Geita kwa kuendelea kuwekeza nguvu ya kuchochea maendeleo kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani.
