Storm FM

DC Geita ashiriki uzinduzi wa MMU ya ulipuzi wa miamba migodini

22 June 2026, 4:24 pm

Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa MMU. Picha na Ester Mabula

“Kwanza niwapongeze sana sana ESAP kwa uthubutu huu na hii inaendana sambamba na dhamira ya serikali ya awamu ya sita kuweka mazingira wezeshi kwa wazawa katika mnyororo wa thamani ya madini nchini” – DC Geita Hashim Komba

Na: Ester Mabula

Kampuni ya ESAP Mining Services Limited leo Juni 22, 2026 imezindua rasmi mtambo wa MMU (Mobile Manufacturing Unit ) wenye uwezo wa tani 15 na teknlojia ya kisasa zaidi yenye uwezo wa kuzalisha na kuchaji baruti kwa ajili ya shughuli za ulipuaji miamba katika migodi nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo Juni 22, 2026 eneo la soko la dhahabu manipsaa ya Geita, mgeni rasmi Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba ameipongeza kampuni hiyo kwa uwekezaji huo, akisema ni hatua kubwa katika sekta ya madini nchini huku akieleza dhamira ya serikali ni kuendelea kuwawezesha na kuwasimamia wazawa ili kuwa sehemu ya mnyororo wa thamani ya madini nchini.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba

Aizungumza  Mkurugenzi wa kampuni ya ESAP  Mhandisi Yahya Rashid Puyaga amesema mtambo huo umegharimu zaidi ya shilingi milioni 700 akieleza hatua hiyo ni mkakati wa kampuni wa kujiimarisha ili kukidhi mahitaji ya soko la huduma za vilipuzi migodini.

Sauti ya mkurugenzi wa ESAP Mhandisi Yahya Puyaga
Mkurugenzi wa ESAP Mhandisi Yahya Puyaga akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani). Picha na Ester Mabula

Kwa upande wake mwakilishi wa RMO Geita, Adisa madini mkazi amesema Tume ya madini itaendelea kuwapa ushirikiano katika utendaji wao wa kazi huku Kaimu Kamanda wa Jeshi la zimamoto na uokoaji mkoa wa Geita Keneth Mwakasitu amesema mtambo huo utapunguza ajali zitokanazo na ulipuzi wa miamba.

Sauti ya Afisa madini mkazi na Kaimu Kamanda wa zimamoto Geita
Mtambo wa MMU uliozinduliwa leo na ESAP kwaajili ya shughuli za ulipuaji wa miamba migodini. Picha na Ester Mabula