Storm FM

Mvua yaua watoto wa familia moja Geita

15 April 2024, 3:11 pm

Wakazi wa Kijiji cha Nyakabale Geita wakiwa katika maziko ya watoto wawili wa familia moja. Picha na Mrisho Sadick

Watoto mkoani Geita wamekuwa wahanga huku wengine wakipoteza maisha kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.

Na Mrisho Sadick – Geita

Watoto wawili wa familia moja katika kijiji cha Nyakabale Kata ya Mgusu wilayani na Mkoani Geita wamefariki dunia baada ya kusombwa na maji wakati wakitafuta kuni katika pori la kijiji hicho.

Baba mzazi wa watoto hao Samweli Chacha amewataja waliofariki kuwa ni Ester Samweli mwenye umri wa (14) na Rose Samweli umri wa miaka (9)  ambapo amesema umauti umewakuta baada ya kusombwa na maji  wakati wakiwa porini wakitafuta kuni.

Sauti ya Baba wa watoto waliofariki
Baadhi ya wakazi wa Nyakabale wakiwa katika maziko ya watoto wawili wa familia moja. Picha na Mrisho Sadick

Katibu tawala wa wilaya ya Geita Lucy Beda akiwa katika msiba huo amewaomba wananchi wilayani humo kuendelea kuwalinda watoto kwa kuacha kuwaagiza katika nyakati hizi za mvua zinazoendelea kunyesha ili kuepuka madhara makubwa zaidi.

Mkuu wa wilaya ya Geita Hashimu Komba amesema serikali itaendelea kuboresha miundombinu ambayo imekuwa sababu ya wananchi kukumbwa na mafuriko huku akiwaomba wananchi kuendelea kuwa makini wakati huu wa mvua zinazoendelea kunyesha.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Geita
Mkazi wa Nyakabale akitumia mtumbwi kutoka katika makazi yake yaliyoathiriwa na mvua. Picha Mrisho Sadick