Storm FM

TMDA yaendelea kuelimisha wananchi matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba

30 September 2023, 9:03 pm

Banda la TMDA katika maonesho ya 6 ya kimataifa ya teknolojia ya madini Geita. Picha na TMDA

Matumizi mabaya ya dawa na vifaa tiba bado imeonekana ni changamoto kwa baadhi ya maeneo kanda ya ziwa, hili limesababisha TMDA kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya dawa.

Na Zubeda Handrish- Geita

Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) wa Kanda ya Ziwa Dkt Edgar Mahundi, amewataka watanzania kuendelea kuwa makini na matumizi ya dawa na vifaa tiba kwa kuhakikisha kuwa zinakidhi ubora wa matumizi. 

Ameyasema hayo alipozungumza na Storm FM katika maonesho ya 6 ya teknolojia ya madini katika banda la mamlaka hiyo yaliyokamilika leo Septemba 30, 2023 katika viwanja vya EPZA, Bombambili, kata ya Buhalahala mkoani Geita.

Amesema lengo la mamlaka ya dawa na vifaa tiba kanda ya ziwa kushiriki katika maonyesho hayo ni kutoa elimu kwa wananchi juu ya masuala ya matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba ili wawe na uelewa wa kutumia dawa kwa mujibu wa taalamu wa afya.

Banda la TMDA katika maonesho ya 6 ya kimataifa ya teknolojia ya madini Geita. Picha na TMDA

Ameongeza kuwa wapo wafanyabishara wasio waaminifu ambao wamekuwa wakiuza bidhaa za dawa na vifaa tiba ambavyo havikidhi ubora unaohitajika kadhalika kutoa dawa bila ya kufuata utaratibu wa kitabibu.

Sauti ya Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) wa Kanda ya Ziwa Dkt Edgar Mahundi

Aidha ameongeza kuwa mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera inajirahidi katika matumizi sahihi ya dawa licha ya changamoto zilizopo ambazo serikali inaendelea kushughulikia, na kutoa rai kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa watoa huduma wanaovunja utaratibu.

Aidha mamlaka hiyo ya dawa na vifaa tiba imesema kuwa itaendelea na operesheni zake katika maeneo mbalimbali kukagua kama dawa na vifaa tiba vinavyouzwa madukani vimekidhi viwango vya ubora unaohitajika hapa nchini na itachukua hatua kwa wafanyabishara watakaobainika kuuza dawa hizo, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya dawa, vifaa tiba na vitindanishi.