Storm FM

Shida ya maji, fisi vyawatesa wakazi kijiji cha Lubando

2 November 2023, 5:42 pm

Mkazi wa kijiji cha Lubando akiteka maji katika chanzo cha maji cha asili kilichopo katika kijiji hicho. Picha na Mrisho Sadick

Ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, tishio la fisi vijijini katika wilaya ya Nyang’hwale umeendelea kuwapa changamoto wananchi wanaoishi maeneo hayo ambao huchangia maji na mifugo huku wakitembea umbali wa kilomita 20 kufuata maji.

Na Mrisho Sadick – Geita

Wakazi wa kijiji cha Lubando wilayani Nyang’hwale mkoani Geita wanalazimika kuchangia maji na wanyama kwa kuwa eneo hilo halina chanzo cha uhakika cha maji safi huku wakiiomba serikali kuwachimbia kisima cha kina kirefu ili kuepuka magonjwa pamoja na kushambuliwa na wanyama aina ya fisi wanapokuwa wakitafuta huduma hiyo vijiji jirani.

Wakizungumzia changamoto hiyo baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema wanalazimika kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 20 kutafuta huduma hiyo vijiji jirani hali ambayo inahatarisha usalama wa maisha yao kutokana na uwepo wa wanyama wakali aina ya fisi.

Sauti ya wakazi wa kijiji cha Lubando
Wakazi wa kijiji cha Lubando wakitoka kuteka maji. Picha na Mrisho Sadick

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Shabaka kilipo kijiji hicho Karimu Chasama amesema changamoto ya maji katika eneo hilo ameiwasilisha katika baraza la madiwa la halmashauri hiyo huku akiikumbusha serikali kutatua changamoto hiyo kwani wananchi hao wanaathiri kutokana na kutumia maji machafu.

Akizungumza kwa njia ya simu meneja wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini RUWASA wilaya ya Nyang’hwale Mhandisi Moses Mwampunga amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo katika kijiji hicho nakwamba kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025 itakwenda kumaliza changamoto hiyo.

Sauti ya meneja RUWASA Nyang’hwale