Storm FM

Auawa akidaiwa shilingi elfu 5 Geita

30 August 2023, 12:49 pm

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Geita, ACP Safia Jongo. Picha na Amon Bebe

Matukio ya vijana kudhuriana wao kwa wao kwasababu ya pesa yanaongezeka siku hadi siku, hiyo imepelekea ACP Safia Jondo kuwashauri wazazi kufuatilia mienendo ya vijana wao na watu wao wa karibu.

Na Amon Bebe- Geita

Kijana mmoja mkazi wa mtaa wa Katundu mjini Geita anaefahamika kwa majina ya Lukumani Abubakari amefariki dunia baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali (Kisu) na rafiki yake wakiwa katika mzozo wa kudaiana shilingi Elfu tano katika machinjio ya Mpomvu wilayani na mkoani Geita.

Kijana aliyefariki anaefahamika kwa jina la Lukumani Abubakari

Wakizungumzia tukio hilo baadhi ya ndugu wa marehemu wamesikitishwa na tukio la kumpoteza kijana wao wakisema ilikuwa ni ugomvi na rafiki yake ambaye walikuwa wakifanya nae kazi moja ya kuchuna wanyama katika eneo hilo la machinjio, lakini wakati wa kugawana ujira wao walipishana kauli ndipo mwenzake akachukua maamuzi ya kumchoma kisu.

Sauti ya ndugu wa marehemu wakizungumzia tukio hilo

Nao baadhi ya wananchi wamelaani tukio hilo nakuiomba serikali kijana aliefanya kitendo hicho kuchukuliwa hatua kali za kisheria ili liwe funzo kwa wengine.

Naye mwenyekiti wa mtaa wa katundu Gidion Ally amekiri kupokea taarifa za tukio hilo.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Geita, ACP Safia Jongo amesema marehemu alichomwa kisu kifuani mara mbili na mtuhumiwa huyo mpaka sasa bado wanaendelea kumshikilia kwa hatua zaidi.

Sauti ya Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Geita, ACP Safia Jongo 

Hata hivyo amewaomba wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao na kutambua shughuli wanazofanya na makundi ya watu wanaoambatana nao kama marafiki.