Storm FM

Ugonjwa usiojulikana waua watoto wawili Geita

23 April 2024, 10:16 am

Amina Athuman Jirani wa familia iliyopoteza watoto wawili baada ya kuugua kuharisha na kutapika. Picha na Kale Chongela

Serikali kupitia Wizara ya Afya nchini imeendeleza ajenda ya kuhamasisha jamii kuzingatia kanuni bora za kiafya ikiwemo matumizi ya vyoo bora, kunawa mikono nyakati muhimu na kutunza mazingira ili kujilinda na magonjwa ya kuharisha na kutapika.

Na Kale Chongela – Geita

Watoto wawili wa familia moja katika mtaa wa Uwanja uliopo kata ya Nyankumbu mjini Geita wamefariki dunia baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa kuharisha na kutapika.

Akizungumzia sakata hilo dada mlezi wa watoto hao Bi. Ester James amesema tukio hilo limetokea kwa nyakati tofauti tofauti na kwamba alianza kumpatia dawa ya tumbo mtoto mmoja baada ya kutapika kwa muda mrefu.

Sauti ya dada mlezi akisimulia

Watoto waliofariki wametambulika kwa majina Modrick Stephano (3.5) na Kelvin Stephano (12) aliyekuwa anasoma darasa la sita katika shule ya msingi Uwanja ambapo mama mzazi wa watoto hao naye yupo hospitalini kwa matibabu zaidi.

Mmoja wa majirani Bi. Amina Athuman ameelezea namna alivyokuta jirani yake akilalamika juu ya maumivu anayopitia mara baada ya kufika nyumbani kwake.

Sauti ya Amina Athuman

Sehemu ya mazingira yanayozunguka nyumba waliyokuwa wakiishi watoto waliofariki kutokana na maradhi ya kuharisha na kutapika. Picha na Kale Chongela

Dkt. Sande Mwakyusa ni Mganga Mkuu wa hospitali ya mji Geita amethibitisha vifo vya watoto hao huku akisisitiza wananchi kufanya usafi maeneo yanayowazunguka sambamba na kuzingatia kanuni mbalimbali za afya ikiwemo matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono kwa nyakati muhimu.

Sauti ya Mganga mkuu wa Hospitali ya mji Geita

Mkuu wa wilaya ya Geita Hashimu Komba ameagiza  wananchi kuchukua tahadhari ya kutumia maji safi na salama pamoja na kuagiza wakurugenzi wa Halamsahauri zotembili ikiwemo Mji pamoja na wilaya kutenga vikusanya taka katika Maeneo yao.

Sauti ya mkuu wa wilaya ya Geita