Storm FM

Moto wa ajabu wateketeza Nyumba

12 December 2022, 2:54 pm

        Inspekta  Edward Lukuba

Jeshi la zimamoto na uokoaji Mkoani Geita limewataka wananchi kuendelea kutumia namba ya 114 kwa ajili ya kutoa taarifa za majanga ya moto na matukio yanayohitaji uokozi haraka kwakuwa wengi wao wamekuwa wakitoa taarifa pindi tatizo linapokuwa kubwa.

Rai hiyo imetolewa na kaimu kamanda wa jeshi la Zimamoto na uokoaji Mkoani Geita Inspectar Edward Lukuba kufuatia tukio la moto kuteketeza nyumba ya Bw John Magunguli na samani zote za ndani katika Mtaa wa shilabela mjini Geita ambapo chanzo cha tukio hilo kinahusishwa na chuki baina ya majirani na mpangaji aliyekuwa amepanga katika nyumba hiyo Bi Adelina Hamis.

Bi Adelina  Hamisi ameiambia Storm FM kuwa akiwa usingizini majira ya saa nane usiku alishituka ghafla nakuona godoro likiwa linawaka moto akaanza kuomba msaada kutoka kwa majirani  licha ya jitihada za kuuzima moto  huo wenyewe hawakufanikiwa na wakashindwa nini wafanye ili kulipata jeshi la zimamoto na uokoaji.

Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa shilabela Bw Fedrick Masalu  amesema baada ya kupewa taarifa alifika katika nyumba hiyo na kwamba hatua za awali zilizobainika ni kwamba kulikuwa na tundu kutokea nje ya nyumba kitu ambacho kimetajwa huenda likawa tukio lakupangwa na watu ambao hawajafahamika mpaka sasa.

Vitu vilivyoteketea katika nyumba hiyo vimekadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi Milioni moja, huku Jeshi la zimamoto na uokoji Mkoani Geita limefika eneo la tukio na linaendelea na uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha tukio hilo.