Storm FM

Mkuu wa wilaya Chato atoa onyo kwa waharibifu shamba la miti Silayo

6 September 2023, 10:49 pm

Uwepo wa Shamba la Miti Silayo wilayani Chato ni manufaa makubwa kwa wakazi wa eneo hilo kulingana na namna linaendelea kurudisha kwa jamii licha ya changamoto kadha wa kadha katika kulilinda shamba hilo.

Na Zubeda Handrish- Geita

Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale ametoa onyo kwa waharibifu na wasiolitakia mema Shamba la Miti Silayo lililopo katika kata ya Butengolumasa, wilayani Chato, mkoani Geita.

Ameyasema hayo jana Septemba 5, 2023 wakati wa kutoa msaada wa madawati 50 kwa shule ya msingi Nyamibanga na Butengo na viti 30 kwa walimu shule ya sekondari Bwanga.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale

Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya Katwale amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakaebainika anahusika na kukata miti kwaajili ya biashara ya mkaa kinyume cha sheria.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Chato Deusdedith Katwale

Akisoma taarifa juu ya shamba hilo Mhifadhi Mkuu Mwandamizi Shamba la Miti Silayo Juma Mwita Mseti amesema moja ya changamoto inayolikumba shamba hilo ni ukataji wa miti kiholela huku akiiomba kamati ya wilaya kutoa ushirikiano kuikabili changamoto hiyo.

Sauti ya Mhifadhi Mkuu Mwandamizi Shamba la Miti Silayo Juma Mwita Mseti

Nao baadhi ya wananchi wamezungumzia changamoto hiyo wakiwasihi wanaokata miti kwaajili ya mkaa katika shamba hilo waache.

Sauti za baadhi ya wakazi wa wilaya ya Chato

Shamba la miti Silayo ni miongoni mwa mashamba 24 ya serikali yanayosimamiwa na kuendelezwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) likianzishwa Januari 27, 2021 na lina ukubwa wa hekta 64,040 baada ya hekta nyingine kumegwa kwaajili ya wananchi, likiwa ni la pili kwa ukubwa baada ya Shamba la Miti la Saohill lililopo Mafinga mkoani Iringa, likijumuisha msitu wa asili na eneo la upandaji miti.