Storm FM

Sakata la Mpanduji kujiua, wananchi wawakataa viongozi wa kijiji

29 April 2024, 5:31 pm

Mkuu wa wilaya ya Chato Said Nkumba. Picha maktaba na Storm FM

Baada ya Storm Fm kuripoti taarifa ya mwanaume mmoja Mpanduji Mshigwa (46) mkazi wa kijiji cha Busaka kata ya Bwera halmashauri ya Chato kujiua kwa kile kilichodaiwa kuingia mgogoro na mwanaume aliyetambulika kwa jina moja la Halawa (mganga wa jadi) aliyetembea na mke wake na kumzalisha mtoto mmoja na pia akimpa ujauzito mwingine, wananchi wamewakataa viongozi wa kijiji kwa kushindwa kutatua migogoro ya wananchi.

Na: Evance Mlyakado – Geita

Wananchi wa kijiji cha Busaka kata ya bwera halmashauri ya Chato wamefikia uamuzi wa kuwaondoa madarakani viongozi watatu  wa kijiji hicho kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Wakizungumza na Storm fm wananchi hao wamesema uamuzi huo umefikiwa katika kikao kilichoketi kando ya msiba wa Mpanduji Mshigwa mara tu baada ya shughuli ya kumpumzisha mpendwa wao kukamilika ambapo viongozi walioondolewa ni Mwenyekiti wa kijiji hicho, Mwenyekiti wa CCM kata na Afisa mtendaji wa kijiji hicho.

Sauti ya wananchi wa kijiji cha Busaka

Diwani wa kata hiyo Masumbuko Manyenye amesema kuhusu uamuzi wa wananchi hawezi kueleza lolote huku akikemea tabia ya wananchi kujihusisha na vitendo vya uzinzi kijijini hapo kwani ndio sababu kuu iliyopelekea kutokea kwa tukio hilo.

Sauti ya Diwani wa kata ya Bwera

Kwa Upande wake mkuu wa wilaya ya chato Bw. Said Nkumba amethibitisha kuufahamu mgogoro huo na hivyo kuahidi kufika katika kijiji hicho kwa lengo la kuzungumza na wananchi ili kufahamu namna bora ya kutatua mgogoro huo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Chato

Hatua ya wananchi kuwaondoa viongozi hao madarakani inaelezwa ni kutokana na kushindwa kushughulikia mgogoro wa Bw. Halawa ambaye alikuwa akitembea kimahusiano na mke wa Mpanduji Mshigwa (marehemu kwa sasa) hali iliyompelekea Bw. Mpanduji kujitoa uhai kwa kujichoma kisu tumboni.