Storm FM

TBA yaupiga mwingi mradi wa majengo mkoa wa Geita

29 September 2023, 12:34 pm

Meneja wa TBA mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jefta. Picha na Zubeda Handrish

Na Zubeda Handrish- Geita
Wakala wa majengo Tanzania (TBA) kupitia kwa Meneja wa TBA mkoa wa Geita Mhandisi Gladys Jefta Septemba 28,2023 amesema awamu ya kwanza (phase one) ya ujenzi wa majengo saba ya serikali  katika Mkoa wa Geita imekamilika ambapo miradi hiyo imetekelezwa katika wilaya za Nyang’hwale, Mbogwe, Chato na Geita.

Jefta amesema katika banda lao kwenye maonyesho ya kimataifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya EPZA Mjini Geita wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Mhandisi Jefta ametaja majengo hayo kuwa ni pamoja majengo ya ofisi ya mkuu wa mkoa wa Geita, majengo ya Hospitali ya rufaa ya Kanda ya Chato, majengo ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale na Mkuu wa Wilaya Mbogwe.

Miradi mingine ni majengo ya ofisi za Shirika la umeme nchini (TANESCO) za Wilaya ya Chato na wilaya ya  Geita.

Jengo la ofisi ya mkuu wa mkoa

Hata hivyo amesema kuwa mradi mwingine unaoendelea kujengwa ni majengo ya makazi ya mkuu wa mkoa, hazina ndogo ambayo TBA ni mkandarasi mshauri katika mradi huo na upanuzi wa jengo la ofisi za mamlaka ya mapato Tanzania (TRA).

Aidha ameeleza kuwa TBA iko kwenye hatua za mwanzo za kukamilisha taratibu za kuanza kujenga nyumba za makazi za watumishi wa umma katikati ya mji baada ya mabadiliko ya sheria ya hivi karibu.

TBA inashiriki maonesho ya sita ya teknolojia ya madini katika viwanja vya EPZA mjini Geita yaliyoanza Septemba 20 ,2023 na kufunguliwa rasmu na Naibu Waziri Mkuu Dr. Doto Biteko Septemba 23,2023 na yanatarajiwa kufungwa rasmi na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kesho Septemba 30, 2023.