Storm FM

GGML yapewa ruhusa uchimbaji wa wazi

21 April 2021, 10:46 am

Na Joel Maduka:

Kampuni ya uchimbaji wa madini ya Anglo Gold Ashanti Kupitia mgodi wake wa Geita Gold Mining Limited (GGML) imepokea ruhusa ya mpango wa uchimbaji madini wa mwaka 2021 unaohusisha uchimbaji wa wazi na wa chini kwa chini kwenye  eneo la Nyamulilima lililopo Kata ya Mgusu wilayani Geita.

Mkaguzi Mkuu wa Migodi yote nchini Dkt Abdul Rahman Mwanga ameruhusu mpango huo baada ya GGML kupeleka nyaraka zote Tume ya Madini na kupatiwa vibali.Kufuatia ruhusa hiyo, GGML sasa inatarajiwa kufanya shughuli zake za uchimbaji  kwenye  eneo hilo na akizungumza wakati wa uzinduzi wa shughuli za uchimbaji ,Kaimu meneja wa Mgodi wa GGML Wayne Lauw,ameelezea namna ambavyo mgodi huo umeendelea kufanya vizuri kwenye masuala mbali mbali ya kiuchimbaji.

Afisa mwendeshaji Mkuu wa Anglo gold ashant Sicelo Ntuli amesema kuanza kwa mradi kutasaidia kupata Tani Milioni Tano kwa Mwaka kutokana na kinu ambacho kitakuwa kikitumika huku Makamu wa Mgodi wa GGM,Saimon Shayo ameelezea jitihada ambazo mgodi wamekuwa wakizifanya kurudisha uoto wa asili pindi wanapomaliza uchimbaji.

Hivi karibuni GGML iliibuka mshindi wa jumla wa kampuni zinazofanya vizuri kwenye sekta ya madini  nchini Tanzania kwa mwaka 2019/2020. GGML iliibuka mshindi katika vipengele vya Wajibu wa  Kampuni kwa Jamii (CSR), Utunzaji mazingira na usalama, ukusanyaji wa mapato ya Serikali (kodi)  pamoja na uwezeshaji wa wazawa.