Storm FM

Wananchi zaidi ya 200 wamejitokeza kupima afya na GGML

30 April 2024, 6:49 pm

Daktari wa GGML aliyebobea katika magonjwa yatokanayo na kazi, Cretus Karwan akimpatia vipimo mmoja wa wananchi waliotembelea banda la GGML. Picha na Gabriel Mushi

Watu wengi hawazingatii usalama mahala pa kazi hali ambayo inawafanya kupata madhara ikiwemo ya kiafya yanayowafanya kushindwa kuendelea na kazi.

Na Mwandishi wetu:

ZAIDI ya watu 200 jijini Arusha wamejitokeza kupimwa afya na Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) na kati yao kubainika kuwa wana tatizo la uzito uliopitiliza.

Pia kati ya watu hao hakuna aliyebainika kuwa na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), lakini mmoja amekutwa na dalili zote za kifua kifuu hivyo kupewa rufaa ya kwenda katika Hospitali ya Mount Meru iliyopo mkoani humo.

Hayo yamebainishwa na Daktari wa GGML aliyebobea katika magonjwa yatokanayo na kazi, Cretus Karwan alipozungumza na mwandishi wetu kuhusu huduma za afya zilizokuwa zinatolewa kwenye banda la GGML katika maonesho ya afya na usalama kazini (OSHA) 2024 yaliyofanyika jijini Arusha.

Alisema katika banda hilo wameendelea kupima uzito, urefu na magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, shinikizo la damu, VVU na magonjwa mengine.

“Mathalani kuna binti mmoja tulimpima tukakuta presha na sukari yake imeshuka na tulibaini ni kutokana na kwamba kutokula kwa wakati. Alikuja mchana hivyo tulimpa huduma ya kwanza na kumshaui aende kunywa supu na maji mengi,” alisema.

Alisema pamoja na mambo mengine washiriki au wananchi waliotembelea banda la GGML pia walijifunza namna kampuni hiyo inavyotoa huduma za afya kwa wanyakazi wake.

“Washiriki au wateja wetu tuliwaeleza tunachofanya tunapokuwa kazini. Tuliwaeleza tunamfanyia vipimo mfanyakazi anapoajiriwa kujua kwamba kwa kazi aliyoajiriwa anaimudu au lah kulingana na afya yake kabla ya kufanya kazi na GGML.

Hivyo tunampima pia kuainisha uzito na urefu ulivyo na kumshauri,
“Tunapima masikio, macho, kifua na vitu vingine kujua yuko sawa au lah. Hivi ni vipimo ambavyo kila mwaka huwa tunarudia,” alisema.

Pia alisema huwa wanapima eneo la kazi la mfanyakazi kujua kama kiwango cha kelele kimezidi, vumbi na vitu vingine ili kujua kama mfanyakazi ameathirika.
“Haya ni matakwa ya kisheria kwamba mtu anapofanya kazi katika mazingira fulani tunamdhibitishia ameathirika au lah na wao wanakuwa na amani.

“Hii inatusaidia kwa sababu mtu akiacha kazi, au kustaafu pia tunampima ambapo yeye binafsi anajua tangu alipoingia mgodini ameathirika na tatizo lolote au lah lakini pia na mgodi unajua ameondoka yuko vizuri au lah,” alisema.

Alisema iwapo mfanyakazi akikutwa na tatizo lolote anaelekezwa sehemu husika ambapo ni mfuko wa fidia kwa wafanyakazi hivyo mtu huyo anafaidika.

Mwananchi akiwa kwenye banda la GGML akipatiwa huduma za awali za upimaji wa afya katika maonesho ya OSHA yanayoendelea jijini Arusha. Picha na Gabriel Mushi

Mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata huduma za afya kwenye banda hilo, Mussa Abdalah aliishukuru kampuni hiyo kwa kutoa huduma hizo kwani mbali na wananchi kupata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu afya na usalama mahali pa kazi, pia imekuwa fursa kwao kujua hali ya afya zao bure.

“Hivi ni vipimo vya bure kabisa, ukienda hospitali lazima mfuko utoboke lakini hapani bure. Kwa kweli tunashukuru sana kwa huduma hii,” alisema Abdallah ambaye ni mkazi wa Moshono mkoani humo.

Mwananchi akiwa kwenye banda la GGML akipatiwa huduma za awali za upimaji wa afya katika maonesho ya OSHA yanayoendelea jijini Arusha. Picha na Gabriel Mushi