Storm FM

Kampuni ya utafiti wa madini yakana kuwalipa fidia wananchi kupisha maeneo yao.

4 April 2021, 2:21 pm

KAMPUNI ya Utafiti wa madini ya Mabangu  imekana  kuzilipa  fidia ya mashamba   familia 22 za wakazi wa kijiji cha Nyakafulu wilayani Mbogwe mkoani Geita ili kupisha shughuli za uchimbaji na badala yake imesema malipo iliyowalipa yalikuwa ni kwa ajili ya Usumbufu wa utafiti  katika maeneo yao.

Akizungumzia hatua hiyo Meja Mstaafu, Bahati Matala  ambae ni Mshauri wa mahusiano  ya Jamii wa Kampuni  ya Mabangu  amesema kampuni hiyo imelazimika kutoa ufafanuzi kutokana na sintofahamu iliyoibuka  kati ya Serkali ya wilaya ya Mbogwe na  Familia  hizo 22 baada ya  Serkali ya wilaya ya Mbogwe kuzizuia familia hizo kunufaika na uzalishaji  wa madini  ya dhahabu yanayopatikana katika mashamba yao.

Miongoni mwa watu wanaodai kuwa ndio wamiliki halali wa mashamba hayo wamesema  malipo yaliyofanywa na kampuni ya mabangu yalikuwa ya usumbufu  wa kuruhusu kufanyika utafiti katika mashamba yao na siyo fidia ya kupisha shughuli za uchimbani nakwamba kinachofanyika kwasasa nikuminya haki zao.

Martha Mkupasi Mkuu wa wilaya ya Mbogwe  hivi karibuni  akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake alisema  Serikali ya wilaya imezizuia familia  hizo 22 kunufaika na uzalishaji  wa madini ya dhahabu unaopatikana katika mashamba  hayo  kwa madai kuwa walishalipwa fidia na kampuni ya Utafiti  Madini ya  Mabangu ili kupisha shughuli za uchimbaji.