Storm FM

Watu 8 hufariki kila mwezi kwa TB Geita

8 July 2023, 3:57 pm

Waandishi wa Habari Mkoa wa Geita wakifuatilia mafunzo.Picha na Mrisho Sadick

Ugonjwa wa kifua kikuu (TB) umeendelea kuwa tishio mkoani Geita kutokana na idadi ya watu wanaobainika kuwa na ugonjwa huo kwa mwaka pamoja na idadi ya watu wanaofariki dunia.

Na Mrisho Sadick- Geita

Watu wanane (8) wanafariki dunia kila mwezi kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu mkoani Geita huku mikakati ya kupunguza vifo hivyo ikiendelea kwa kuwaibua wagonjwa wapya na kuwaweka kwenye matibabu haraka.

Takwimu hizo zimetolewa na mratibu wa kifua kikuu na ukoma mkoani Geita Dkt. Michael Mashala katika semina ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari juu ya ugonjwa huo ambapo amesema kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka huu wamefanikiwa kuwafikia wahisiwa wa ugonjwa huo 1,122 huku malengo ya kitaifa yakiwa ni kuwafikia wahisiwa zaidi ya 4,400.

Dkt. Mashala amesema ugonjwa huo unaenezwa kwa wingi kwenye maeneo ya migodi ya wachimbaji wadogo, kambi za wavuvi , magerezani pamoja na kwenye mabweni na kwamba jitihada mbalimbali zinafanyika kuhakikisha wanawapata wahisiwa wengi ili wawekwe kwenye matibabu wasiendelee kuwaambukiza watu wengine.

Sauti ya Mratibu wa Kifua Kikuu Mkoa wa Geita Dkt Michael Mashala
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Geita Dkt Michael Mashala. Picha na Mrisho Sadick

Mafunzo hayo yameandaliwa na serikali kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la AMREF pamoja na umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini UTPC huku Mkurugenzi Mtendaji wa umoja huo Keneth Simbaya akizungumzia mikakati ya kuisaidia serikali katika mapambano dhidi ya TB.

Sauti ya Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya
Mkurugenzi Mtendaji wa UTPC Kenneth Simbaya akizungumza kwenye Mafunzo.Picha na Mrisho Sadick