Wananchi walia na mikopo kausha damu Katoro
16 May 2024, 9:58 am
Mkuu wa wilaya ya Geita Mhe. Hashim Komba ameendelea na ziara ya kutembelea wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya yake ili kusikiliza kero zao.
Na: Edga Rwenduru – Geita
Baadhi ya wakazi wa mamlaka ya mji mdogo wa katoro mkoani Geita wamelalamikia kitendo cha nyumba zao kuuzwa bila wao kushirikishwa na watu wanaofanya biashara ya mikopo ya kausha damu hali ambayo imepelekea wengi wao kubaki bila makazi licha ya kulipa mikopo hiyo.
Wamebainisha wakati wa mkutano wa adhara wa mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba uliofanyika katika eneo hilo ambapo wamesema walichukua mikopo hiyo kwa nyakati tofauti kwa mtu anayefahamika kama Kapaya Emmanuel kuanzia mwaka 2012 lakini hadi sasa hawajapatiwa hati za nyumba zao.
Mwakilishi wa Kapaya Emmanuel ambaye anatuhumiwa kuuza baadhi ya nyumba za wananchi hao Janeth Barahigima amesema yeye hatambui chochote juu ya madai hayo kwani wakati mkopeshaji anawakopesha alikuwa bado hajafungua kampuni ya ukopeshaji
Mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba amesema taasisi za mikopo zipo kwa mujibu wa sheria lakini wamiliki wamekuwa wakikiuka sheria hizo ikiwemo kuanza biashara ya kukopesha bila kuwa na kibali huku akimsimamisha Kapaya Emmanuel kuendelea na shughuli hiyo mpaka mei 28, 2024 watakapokaa pamoja kusuluhisha changamoto hiyo.