Storm FM

Ubovu wa barabara wakwamisha huduma za kijamii Songambele

8 April 2024, 9:59 pm

Mwendesha bodaboda pamoja na abiria wake wakihangaika kuvuka katika moja ya eneo ambapo barabara imeharibiwa na mvua. Picha na Kale Chongela

14 Kambarage ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaendelea kushuhudia athari za mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo tofautitofauti ya mkoa wa Geita na nchi nzima kwa ujumla.

Na kale Chongela

Wakazi wa Songambele mtaa wa 14 Kambarage kata ya Buhalahala mjini Geita  wamedai kukabiliwa na changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara hali ambayo inakwamisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa urahisi.

Mojawapo ya barabara iliyoharibiwa na mvua kutoka mtaa wa 14 kambarage. Picha na Kale Chongela

Baadhi ya wakazi wa  Songambele wamesema ubovu huo wa barabara unapelekea baadhi ya maji kuingia kwenye nyumba za watu kutokana na barabara hizo kukosa mitaro ya kusafirisha maji.

Aidha wananchi hao wameongeza kuwa kutokana na adha hiyo wanalazimika kuvua viatu hasa wakati wa mvua inaponyesha kwani inakuwa vigumu kutembea eneo hilo kutokana na maji kuingia kwenye makazi yao.

Baadhi ya wananchi wa Songambele ndani ya mtaa wa 14 Kambarage

Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini TARURA wilaya ya Geita Mhandisi Bahati Subeya amekiri kuwepo kwa baadhi ya barabara kuharibiwa na mvua na kwamba ili kutatua changamoto hiyo tayari wameshaanza kupokea fedha  za dharura ili kuboresha  maeneo yaliyoharibiwa na mvua.

Sauti ya meneja wa TARURA wilaya ya Geita
Gari likihangaika kupita katika moja kati ya Barabara ndani ya mtaa wa 14 Kambarage. Picha na Kale Chongela