Storm FM
Storm FM
3 August 2026, 12:33 pm

Uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kisasa na una miundombinu muhimu ikiwemo mfumo wa taa za kisasa. Eneo la kuchezea lina nyasi bandia zenye ithibati ya FIFA Daraja la Kwanza, lenye urefu wa mita 105 na upana wa mita 68.
Na Mrisho Sadick:
Klabu ya Yanga SC inatarajiwa kushiriki shamrashamra za Joto la Ligi Kuu zitakazofanyika Wilayani Bukombe mkoani Geita Agosti 4,2026 ikiwa ni sehemu ya utambulisho wa Uwanja mpya wa kisasa wa Bukombe utakaotumiwa na Geita Gold FC katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2026/2027.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, amesema uwanja huo umejengwa na Halmashauri kwa kushirikiana na wadau mbalimbali. Amesema kuwa tarehe 4 Agosti 2026, Yanga SC imethibitisha kushiriki katika tamasha la Joto la Ligi Kuu, litakaloambatana na burudani mbalimbali zitakazoanza tangu asubuhi ya siku hiyo.
Muragili amesema uwanja huo una uwezo wa kuchukua zaidi ya watazamaji 5,000, ambapo zaidi ya 4,000 watakuwa wamekaa kwenye viti. Baada ya Yanga SC kufanya mazoezi katika dimba hilo na kutambulisha baadhi ya wachezaji wa kikosi chake, kutachezwa mechi ya kirafiki kati ya Geita Gold FC na Pamba Jiji FC ya Mwanza.