Storm FM

Nyang’hwale yaanza kuchukua tahadhari ya mvua za El Nino

16 August 2026, 5:50 pm

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame akizungumza kwenye kikao cha Baraza. Picha na Mrisho Sadick

Tahadhari hii inachukuliwa mapema kutokana na mkoa wa Geita kuwa miongoni mwa mikoa ambayo inapata mvua nyingi Tanzania.

Na Mrisho Sadick:

Serikali wilayani Nyang’hwale mkoani Geita imeanza kuchukua tahadhari dhidi ya mvua kubwa za El Nino, huku wananchi wakitakiwa kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kutambua na kutoa taarifa kuhusu maeneo hatarishi ili hatua za haraka zichukuliwe.

Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Robo ya Nne cha Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo amesema kwa mujibu wa utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuna uwezekano wa kunyesha mvua kubwa hivyo Serikali imeanza kuchukua tahadhari mapema ili kunusuru wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.

Viongozi mbalimbali wakiwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani Halmashauri ya Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Kingalame amesema ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika kubaini maeneo hatarishi, ikiwemo maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko na magonjwa ya mlipuko  ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.

Katika kikao hicho taasisi za umma ikiwemo RUWASA, TANESCO na TARURA zimewasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi na majukumu yao katika wilaya hiyo huku kukiwa na mafanikio makubwa.

Madiwani wakiwa kwenye kikao cha Baraza la madiwani Halmashauri ya Nyang’hwale. Picha na Mrisho Sadick

Mwenyekiti wa Halmashauri amewataka watendaji kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuongeza uwajibikaji na kulinda miradi hiyo

Ripoti kamili na Mrisho Sadick