Storm FM
Storm FM
5 September 2026, 1:16 pm

Uwepo wa alama zinazoonekana vizuri ni muhimu katika kuwasaidia madereva na watembea kwa miguu kuchukua tahadhari na hivyo kupunguza uwezekano wa ajali za barabarani.
Na Kale Chongela:
Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Geita imefanya maboresho ya alama za barabarani, ikiwemo alama za vivuko vya watembea kwa miguu hatua inayolenga kuongeza usalama na kurahisisha wananchi kuvuka barabara kutoka upande mmoja kwenda mwingine.
Akizungumza na Storm FM Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita Mhandisi Hosea Machaka amesema maboresho hayo yamefanyika katika maeneo mbalimbali yenye matumizi makubwa ya barabara ambapo alama zilizokuwa zimefifia au kutoonekana vizuri zimeboreshwa.
Amesema hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa tahadhari na usalama kwa watumiaji wote wa barabara hususan watembea kwa miguu wanaotumia vivuko vilivyowekwa katika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Geita wameishukuru TANROADS kwa hatua hiyo wamesema maboresho hayo yameongeza mwonekano wa alama za barabarani katika maeneo ya Mwatulole na Shilabela yaliyopo katika Kata ya Nyankumbu ambazo awali zilikuwa zimefifia.