Storm FM

Akamatwa kwa tuhuma za kuuza kiwanja cha ukoo Geita

12 May 2026, 4:10 pm

Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Mpomvu Manispaa ya Geita Mkoani Geita. Picha na Kale Chongela

Changamoto hiyo ilibainika baada ya mnunuzi wa kiwanja hicho kuanza hatua za ujenzi wa nyumba ndipo familia ikaamua kuchukua hatua

Na Kale Chongela:

Mwanaume mmoja aitwaye Bundala Theonest mkazi wa Mtaa wa Mpomvu Kata ya Mtakuja Manispaa ya Geita amefikishwa katika ofisi ya serikali ya mtaa huo kwa tuhuma za kuuza kiwanja kinachodaiwa kuwa mali ya ukoo bila kufuata taratibu za kifamilia.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mpomvu Kata ya Mtakuja Manispaa ya Geita Charles Manyanga amethibitisha kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo na kueleza kuwa bado anaendelea kufanyiwa mahojiano ili kubaini chanzo cha kuuza kiwanja hicho cha ukoo kwa thamani ya shilingi milioni 1.6.

Sauti ya Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpomvu
Katika picha ni kiwanja cha ukoo kilichodaiwa kuuzwa. Picha na Kale Chongela

Kwa upande wake Balozi wa Shina namba 4 eneo kilipo kiwanja hicho Amos John amesema changamoto hiyo ilibainika baada ya mnunuzi wa kiwanja hicho kuanza hatua za ujenzi ndipo mmoja wa ndugu wa familia kuzuia shughuli hiyo hali iliyosababisha Bundala Theonest kukamatwa na kufikishwa ofisini kwa ajili ya maelezo zaidi.

Akiwa katika ofisi ya serikali ya mtaa huo Bundala Theonest amekiri kuuza kiwanja hicho kwa thamani ya shilingi milioni 1.6 ambapo awali alilipwa shilingi milioni 1.2 na baadaye kukabidhiwa kiasi cha shilingi laki nne zilizokamilisha malipo hayo.

Maamuzi yaliyofikiwa kwenye suala hilo ni mdaiwa kukubali kumrudishia pesa yake mnunuzi wa kiwanja hicho kwa kuweka rehani nyumba yake na fedha hiyo kiasi cha shilini milioni 1 na laki tisa na elfu hamsini ameahidi kuilipa tarehe 30 mwezi wa saba mwaka huu.