Storm FM
Storm FM
30 May 2026, 6:15 pm

GGML imeendeleza dhamira yake ya kuikumbuka na kurejesha kwa Jamii kwa kugusa makundi mbalimbali kupitia ufadhili wa elimu pamoja na vifaa kwa wanafunzi wa kike mkoani Geita.
Na: Ester Mabula
Kampuni ya GGML (Geita Gold Minning Limited) imefadhili jumla ya Pedi 5000 zenye thamani ya shilingi miliion 42 kwa wanafunzi wa kike kutoka katika shule za msingi na sekondari 56 zilizopo mkoani Geita.
Zoezi la ugawaji wa pedi hizo limeendana na utoaji wa elimu kuhusu hedhi salama kwa wanafunzi hao ambalo limefanyika Mei 28, 2026 kwenye ukumbi wa St. Aloysius manispaa ya Geita ikiwa ni maadhimisho ya siku ya hedhi salama.

Akizungumza wakati wa programu hiyo, mwakilishi wa GGML Elibariki Jambau pamoja na mkurugenzi wa GGML Ashraf Suryaningrat wamesema lengo la elimu hiyo ni kuwajengea wanafunzi uelewa sahihi kuhusu hedhi, kuondoa unyanyapaa pamoja na kupunguza utoro kwa wanafunzi wa kike.
Mgeni rasmi, Kamanda wa polisi mkoa wa Geita SACP Safia Jongo ametoa pongezi kwa GGML kwa kuendelea kuimkumbuka Jamii na kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwezesha mazingira bora kwa wanafunzi wote.

Baadhi ya wanafunzi waliopewa elimu hiyo wameeleza kunufaika na kwamba watatumia elimu hiyo kuwaelimisha wazazi na Jamii kuachana na imani potofu juu ya hedhi.

Programu hiyo ni sehemu ya shughuli za kijamii zinazotekelezwa na GGML kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu na afya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira bora ya kujifunza.