Storm FM
Storm FM
18 August 2026, 5:05 pm

Wananchi wametakiwa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi pale wanapobaini vitendo vinavyohatarisha usalama barabarani.
Na Mrisho Sadick:
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Geita limewataka wananchi kutowafumbia macho watu wanaokiuka sheria za usalama barabarani na badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua stahiki zichukuliwe kulinda maisha ya watumiaji wa barabara.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Geita Kamishna Msaidizi wa Polisi Mathayo Msuyale wakati akizungumza na Storm FM kuhusu mikakati ya Jeshi la Polisi ya kukabiliana na vitendo vya uvunjifu wa sheria za usalama barabarani na kupunguza ajali zinazotokana na uzembe.
Kwa upande wao baadhi ya waendesha vyombo vya moto wamekiri kuwa wapo miongoni mwao ambao hawazingatii sheria za usalama barabarani, wakieleza kuwa uzembe huo unachangia kutokea kwa ajali na kuhatarisha maisha ya watumiaji wengine wa barabara.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Geita wamelitaka Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kuongeza nguvu katika kuwabaini na kuwachukulia hatua madereva wanaokiuka sheria kwa makusudi, huku wakisisitiza kuwa usalama barabarani ni jukumu la kila mtumiaji wa barabara.