Storm FM

TASAF yaimarisha huduma za afya kijiji cha Kakora

17 September 2026, 7:03 pm

Jengo la wagonjwa wa nje pamoja na jengo la Baba , Mama na Mtoto katika Zahanati ya Kijiji cha Kakora. Picha na Mrisho Sadick

Kukamilika nakuanza kutoa huduma kwa majengo hayo imekuwa mkombozi kwa wakazi wa kijiji hicho ambao walikuwa wakitembea umbali mrefu kusaka huduma za afya maeneo ya mbali.

Na Mrisho Sadick:

Wakazi wa Kijiji cha Kakora wilayani Nyang’hwale Mkoani Geita wameishukuru serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF kwa kuwajengea  Jengo la wagonjwa wa nje  pamoja na jengo la Baba , Mama na Mtoto  katika Zahanati ya Kijiji  hicho hali ambayo imewaondolea changamoto wananchi.

Wananchi hao wametoa pongezi hizo kwa serikali kupitia mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF  baada ya Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora Mhe Regina Ndege kutembelea nakukagua mradi huo.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF Oscar Maduhu akizungumza na Storm FM.Picha na Mrisho Sadick

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa mfuko wa maendeleo ya Jamii TASAF Oscar Maduhu akiwa katika Ziara hiyo ameipongeza wilaya ya Nyang’hwale kwa kutekeleza miradi 57 ya TASAF ya sekta za Afya na Elimu kwa ubora unaoendana na thamani ya fedha huku Mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale Grace Kingalame akisema miradi hiyo imejengwa kwa zaidi ya Bilioni 2.2.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo afisa mtendaji wa kijiji hicho Joyce Daniel amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi mwaka 2024 kutokana na uhitaji wa jengo la wagonjwa wa nje na jengo la Baba Mama na Mtoto ambapo baada ya kuibuliwa mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF uliwapatia shilingi milioni 92.4 huku jamii ikichangia asilimia 10 ya utekelezaji.

Naibu Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa umma na utawala bora Mhe Regina Ndege akizungumza baada ya kukagua mradi. Picha na Mrisho Sadick

Naibu Waziri Ndege baada ya kutembelea nakukagua mradi huo amewapongeza Wananchi kwa kuanzisha mradi huo kwa nguvu zao kwa kushirikiana na mfuko wa maendeleo Jamii TASAF kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo huku akiwataka kutunza na kulinda mradi huo ili utumike kwa muda mrefu kwakuwa serikali imetumia fedha nyingi kwa ajili yao.

Ripoti kamili ya stori hii na Mrisho Sadick