Storm FM
Storm FM
27 August 2026, 12:10 pm

Kwa mujibu wa Gakala lengo la mradi huo ni kuwawezesha wananchi wa Mbogwe na wilaya jirani kupata huduma bora za afya, zikiwemo huduma za kibingwa, bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Na Mrisho Sadick:
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2026 Wazo Michael Mwang’onda amewahimiza Watanzania kufanya uwekezaji wenye tija katika maeneo yao ili kusaidia kutatua changamoto za huduma za kijamii ikiwemo afya.
Mwang’onda ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Mwenge wa Uhuru katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita ambapo Mwenge wa Uhuru umetembelea , kukagua kisha kuzindua mradi wa Hospitali binafsi ya Gakala.

Ametoa kongole kwa mwekezaji mzawa Bunga Gakala kwa uamuzi wa kuwekeza katika sekta ya afya na kueleza kuwa hatua hiyo ni mfano wa uzalendo na dhamira ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha huduma za kijamii.
Kwa upande wake mwekezaji huyo Bunga Gakala amesema ametumia zaidi ya bilioni 3 katika ujenzi wa Hospitali ya Gakala ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuunga mkono upatikanaji wa huduma bora za afya katika Wilaya ya Mbogwe.

Uwekezaji huo ulianza rasmi Desemba 20, 2024 ambapo awamu ya kwanza ilihusisha ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Jengo la Afya ya Uzazi (RCH), jengo la utawala pamoja na wodi za wanaume na wanawake.
Mradi huo pia unahusisha jengo la mionzi, jengo la kujifungulia kwa wanawake, nyumba za watumishi, jengo la upasuaji, kichomea taka pamoja na shimo maalumu la kutupia kondo la nyuma.