Storm FM
Storm FM
10 May 2026, 4:07 pm

Watumishi wa umma wametakiwa kuzingatia maadili ya kazi, kutunza nyaraka na mali za serikali pamoja na kuwajibika ipasavyo ili kulinda ajira zao.
Na Mrisho Sadick:
Mtumishi wa serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe anayadaiwa kuweka rehani nyaraka za serikali ili apate fedha za kunywa pombe, ni miongoni mwa watumishi 11 waliotimuliwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya kinidhamu yakiwemo utoro kazini, ulevi na ubadhirifu wa fedha.
Mtumishi huyo, Juma Shabani Said, ametajwa kufukuzwa kazi baada ya kukutwa na makosa matatu ambayo ni utoro wa siku 90 kazini, ulevi akiwa kazini pamoja na kuweka rehani nyaraka za serikali ili kupata fedha za kunywa pombe.

Uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe baada ya baraza hilo kujigeuza kamati na kuridhia hatua za kinidhamu dhidi ya watumishi hao wa kada mbalimbali.
Akizungumza baada ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Enock John amesema watumishi waliofukuzwa kazi ni pamoja na Maafisa Watendaji watano, watumishi wa afya wawili, maafisa kilimo watatu na mtumishi mmoja wa maendeleo ya jamii.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe Sakina Mohammed amewataka watumishi wa serikali wilayani humo kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma ili kuepuka hatua kali za kinidhamu.