Storm FM

Waliovunjiwa nyumba zao Isingiro wajengewa mpya

13 June 2025, 11:05 pm

Mkuu wa wilaya ya Geita aliyeshika mkasi akikata utepe wa uzinduzi wa Nyumba za wananchi waliovunjiwa na mtambo wa mgodi. Picha na Mrisho Sadick

Tukio hili liliwashangaza wengi kwani licha ya mtambo huo kuparamia makazi hayo na kuharibika vibaya hakuna mtu hata mmoja aliyepoteza maisha.

Na Mrisho Sadick

Familia nne katika kitongoji Cha Isingiro Kata ya Lwamgasa wilayani Geita Mkoani Geita zilizo vunjiwa makazi yao na mtambo aina ya Bulldozer wa mgodi wa dhahabu wa Buckreef baada ya kuvamia makazi yao usiku wa manane wamekabidhiwa nyumba mpya zilizojengwa na mgodi huo kama sehemu ya fidia.

Akitoa taarifa ya mwenendo mzima wa tukio hilo katika zoezi la kukabidhi nyumba hizo, meneja rasilimali watu wa mgodi wa Buckreef Amelda Msuya amesema mgodi huo umetumia zaidi ya milioni 65 kama fidia ya makazi na matibabu kwa wahanga nakwamba tukio la mtambo huo kuvamia makazi ya watu ilitokea tarehe mbili mwezi wa nne mwaka huu baada ya dereva wa mtambo huo kufurushwa na walinzi wa mgodi usiku wa manane wakati akifanya jaribio la wizi wa mafuta diesel ndipo akaanza kukimbiza mtambo huo hovyo nakuparamia makazi ya watu.

Sauti ya meneja rasilimali watu Buckreef
Mkuu wa wilaya ya Geita Kulia katikati ni meneja rasilimali watu wa Buckreef na kushoto ni katibu tawala wa wilaya ya Geita wakiwa katika ukaguzi wa nyumba hizo. Picha na Mrisho

Baadhi ya wahanga wa tukio hilo Mariam Kasandiko na Sesilia John waliokabidhiwa nyumba hizo wameipongeza serikali na mgodi huo kwa kuchukua hatua za haraka kuwajengea nyumba hizo huku wakieleza namna walivyopata taharuki usiku wa tukio hilo.

Sauti ya wahanga wa tukio
Muonekano wa moja ya Nyumba iliyojengwa na mgodi wa Backreef kufidia nyumba iliyovunjwa na mtambo. Picha na Mrisho Sadick

Akikabidhi nyumba hizo , mkuu wa wilaya ya Geita Hashim Komba ameupongeza Mgodi huo kwa kutekeleza maagizo ya Serikali kwa wakati ya kujenga nyumba hizo huku akiwataka wananchi kuendelea kushirikiana na Mgodi huo kwa kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu na hujuma dhidi ya Mgodi huo.

Sauti ya Mkuu wa wilaya ya Geita