Storm FM
Storm FM
14 May 2026, 11:54 am

“Fedha hizi zimedhibitiwa kwa kipindi cha miezi mitatu na mikakati ya TAKUKURU mkoa wa Geita ni kuendelea kuzuia vitendo vya Rushwa sambamba na mkutoa elimu kwa UMMA juu ya athari za vitendo hivyo” – James Ruge, Mkuu wa TAKUKURU Geita.
Na: Ester Mabula
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Geita kwa kipindi cha mwezi Januari – Machi, 2026 imesaidia kurejesha kiasi cha shilingi 15,816,641 katika udhibiti wa miradi ya maendeleo, chambuzi za mifumo, uchunguzi na mashtaka mbalimbali.
Akizungumza leo Mei 14, 2026 na waandishi wa habari Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Geita James Ruge amesema fedha hizo zimerejesha katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari hadi Machi, 2026.
Akizungumzia uchambuzi wa mifumo amesema, TAKUKURU mkoa wa Geita imefanya chambuzi sita (6) za mfumo ikiwemo uchambuzi wa mfumo wa ulipaji wa ushuru wa huduma kwa wakandarasi/ wazabuni katika Halmashauri ya wilaya ya Chato.
Katika Uchambuzi huu yaliwekwa maazimio matatu ambayo utekelezaji wake umesaidia kiasi cha shilingi 6,814,640.60 kuwasilishwa katika akaunti ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Chato kutoka kwa wakandarasi na wazabuni wanaoshiriki katika utekelezaji wamiradi ya Maendeleo katika Halmashauri hiyo.
Kwa upande wa elimu kwa Umma jumla ya wananchi 13,686 wamepewa elimu kuhusu madhara ya rushwa wakiwemo watumishi wa UMMA, Sekta binafsi, vijana, wanawake na wazee ambapo elimu hiyo imetajwa imesaidia kuhamasisha wadau kuwa na utayari wa kushirikiana na TAKUKURU kuzuia vitendo vya rushwa lakini kuwa tayari kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa ujasiri bila uoga.