Storm FM
Storm FM
10 August 2026, 12:02 pm

Wajumbe wa Kikao cha 17 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Geita wameiomba Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya maboresho ya taa za barabarani wakieleza kuwa taa zilizopo kwa sasa hazina ufanisi unaotarajiwa.
Taa hizo zipo katika barabara zinazosimamiwa na wakala wa barabara Tanzania TANROADS na wakala wa barabara mjini na vijijini TARURA
Na Mrisho Sadick:
Katika kikao hicho miongoni mwa wajumbe walioibua hoja ya kuboreshwa kwa taa za barabarani ni Mbunge wa Jimbo la Geita Mjini Chacha Wambura , Katibu tawala wilaya ya chato Thomas Dime na kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita SACP Safia Jongo wakitaka maboresho ya taa za barabarani kwani zilizopo kwasasa zimekosa ufanisi huku zingine zikiwa zimeharibika.
Akijibu hoja hiyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Geita Hosea Machaka amekiri kuwepo kwa changamoto katika mfumo wa taa hizo na kusema kuwa tayari hatua za kutatua tatizo hilo zimeanza kuchukuliwa.

Katika hatua nyingine Meneja huyo amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 15.19 kwa ajili ya utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara mkoani Geita.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita ambaye pia ni Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskas Muragili, amewataka wahusika kuhakikisha hoja zote zilizojadiliwa katika kikao hicho zinachukuliwa kwa uzito na kufanyiwa kazi kwa wakati.

Muragili amesema utekelezaji wa maazimio na hoja zilizotolewa na wajumbe ni muhimu katika kuboresha miundombinu ya barabara na usalama wa watumiaji wa barabara mkoani Geita.