Storm FM
Storm FM
16 September 2026, 6:41 pm

Manispaa ya Geita TASAF imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 kutekeleza miradi 30 ikiwemo miradi 24 ya elimu na sita ya afya
Na Mrisho Sadick:
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Regina Ndege amesema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kuboresha huduma za msingi kwa wananchi kupitia utekelezaji wa miradi ya afya na elimu huku zaidi ya Shilingi bilioni tano zimetumika kutekeleza miradi 56 katika Halmashauri mbili za Wilaya ya Geita mkoani Geita.
Mhe. Ndege amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua miradi iliyotekelezwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF ikiwemo mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Fadhili Bucha na kueleza kuwa kupitia miradi iliyokamilika TASAF imesaidia wananchi zaidi ya milioni 1.3 huku zaidi ya kaya laki nne zikiwa zimeweza kufikia hatua ya kujitegemea nakwamba katika awamu inayofuata, Mfuko huo unalenga kuhudumia zaidi ya kaya laki tano.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Oscar Maduhu amesema TASAF imeendelea kuwa na manufaa kwa wananchi kwa kusaidia kuboresha huduma za msingi na kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Akieleza utekelezaji wa miradi hiyo katika Halmashauri hizo mbili Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba amesema katika Halmashauri ya Manispaa ya Geita TASAF imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 2.4 kutekeleza miradi 30 ikiwemo miradi 24 ya elimu na sita ya afya huku katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita zaidi ya Shilingi bilioni 2.7 zimetumika kutekeleza miradi 26 ambayo inajumuisha miradi 19 ya elimu na saba ya afya.