Storm FM

RC Geita akemea dhulma ataka haki kwa wananchi

11 September 2026, 4:06 pm

Mkuu wa mkoa wa Geita akizungumza na watendaji wa serikali katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Serikali imewapa viongozi dhamana ya kusimamia ustawi wa wananchi, hivyo hakuna sababu ya kero zinazoweza kutatuliwa katika ngazi za wilaya na mkoa kuendelea kuwaumiza wananchi

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti amewataka watendaji wa serikali na viongozi Mkoani Geita kuhakikisha wanatatua kwa wakati kero zinazowakabili wananchi huku akisisitiza kuwa dhamana waliyopewa na serikali inapaswa kuonekana kupitia huduma na utatuzi wa changamoto za wananchi.

Mnyeti ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na watendaji wa serikali viongozi wa dini pamoja na wawakilishi wa makundi mbalimbali katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.

Viongozi mbalimbali wakiwa katika ukumbi wa mikutano wa mkuu wa mkoa wa Geita katika mkutano wa mkuu wa mkoa. Picha na Mrisho Sadick

Amewataka wakuu wa wilaya na watendaji wengine wa serikali kusimamia ipasavyo utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao, ikiwemo malalamiko yanayohusiana na dhuluma katika maeneo ya uchimbaji wa madini.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Geita

Amesema sekta ya madini ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa Mkoa wa Geita hivyo ni muhimu kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia sheria, haki za wananchi na maslahi ya jamii zinazozunguka maeneo ya migodi.

Viongozi wa dini wakiwa katika mkutano wa mkuu wa mkoa wa Geita katika ukumbi wa mikutano wa ofisi yake. Picha na Mrisho Sadick

Katika hatua nyingine amewataka viongozi kujiandaa mapema kukabiliana na uwezekano wa mvua kubwa za El Niño kwa kuyatambua maeneo hatarishi, hususan yale yanayokumbwa na mafuriko, na kuhakikisha wananchi wanaoishi mabondeni wanaondolewa mapema na kuhamishiwa maeneo salama.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Geita