Storm FM

Ally Hapi atoa maagizo ya ujenzi wa barabara ya Geita Kahama

16 June 2026, 10:19 am

Wakazi wa Kata ya Nyarugusu wilayani Geita kwenye mkutano wa Katibu Mkuu Jumuiya ya wazazi taifa. Picha na Ediga Rwenduru

Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 63 inajengwa kwa zaidi ya Shilingi bilioni 113 na kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi kwa wananchi hususani wachimbaji wadogo wa madini ya dhahabu.

Na Mrisho Sadick:

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa Ndugu Ally Hapi ameitaka Serikali ya mkoa wa Geita kuhakikisha inamsimamia kwa karibu mkandarasi aliyesaini mkataba wa ujenzi wa barabara ya Mtakuja–Nyarugusu–Bukoli hadi Kahama ili aanze kazi hiyo haraka.

Ndugu Hapi ametoa maelekezo hayo Juni 15,2026 katika Kata ya Nyarugusu Wilayani Geita wakati akizungumza na mamia ya wananchi wa eneo hilo kwenye mkutano wa hadhara ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuimarisha Jumuiya hiyo na Chama Cha Mapinduzi.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ni muhimu katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa maeneo hayo, hivyo hakuna sababu ya mradi huo kucheleweshwa baada ya mkandarasi kusaini mkataba.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa Ndugu Ally Hapi akizungumza na wakazi wa Kata ya Nyarugusu wilaya ya Geita. Picha na Ediga Rwenduru

Akizungumza kwenye mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba amesema mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 63 inayojengwa kwa zaidi ya bilioni 113 inayojengwa na kampuni ya The Arab Cotractors utasimamiwa kikamilifu ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa viwango.

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Taifa Ndugu Ally Hapi akisalimiana na viongozi wa CCM Wilaya ya Geita. Picha na Ediga Rwenduru

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Kata ya Nyarugusu wameeleza matumaini yao kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutachochea maendeleo ya kiuchumi kwa kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, kuongeza fursa za biashara na kuboresha huduma za kijamii katika eneo hilo.

Ripoti kamili ya Stori hii na Mrisho Sadick